IFAHAMU SAKRAMENTI YA KITUBIO/UPATANISHO
Maana Sakramenti ya kitubio pia huitwa sakramenti ya Upatanisho, ipo katika fungu la sakramenti za uponyaji. Kuna Sakramenti mbili za uponyaji, kitubio na mpako mtakatifu wa wagonjwa. Dhumuni haswa la Sakramenti ya uponyaji ni kuzirejeshea uhai roho zetu pale zinapougua kwa kutenda dhambi. Yesu ndiye tabibu mkuu wa roho zetu naye yu tayari kututibu kila tunapougua. (Katekisimu Katoliki 1420,1421) Sakramenti ya kitubio huhusisha, kutambua makosa, kujuta na kuungama pamoja na kuweka nia ya kutotenda dhambi hiyo tena. Kitubio hutusafisha dhambi tulizozitenda baada ya ubatizo. Tunakumbuka, siku ya ubatizo tulipewa kitambaa cheupe, ikiwa ni ishara ya kuwa sasa tumekuwa wapya. Lakini kadri tunavyosongwa na mambo ya dunia, kitambaa chetu cheupe kinachafuka nacho chahitaji kusafishwa, ndio maana tunapata Sakramenti ya kitubio. Wakati gani unahitaji Sakramenti ya kitubio Kila wakati unapotenda dhambi unahitaji Sakramenti ya kitubio. Usisubiri ukirundika dhambi zako ili...