UPENDO DHIDI YA HOFU NA WAJIBU


Nishikapo Amri za Mungu, za Kanisa na kufuata miongozo ya viongozi wangu, nafanya kwa sababu ya upendo au nafanya kwa kuwa ninaogopa kuwa nisipofanya nitaonekana ni mkaidi, jamii haitanielewa na sitaingia Mbinguni? Ninapotoa zaka, kuwasaidia masikini na kufanya kazi za Mungu, Je, ninafanya kwa kutimiza wajibu au ninafanya kwa sababu ninampenda Mungu na jirani?

Aghalabu maisha yetu yametawaliwa na hofu juu ya adhabu za Mungu na za jamii na mara nyingi twafanya mambo mengi tukiwa na lengo la kutimiza wajibu wala si kwa sababu ya upendo. Kuishi kwa kuogopa sheria na kufanya mambo mema kwa kutimiza wajibu bila upendo kunachosha na kunaondoa furaha ya jambo zuri tulifanyalo. Lakini pia sifai mbele za Bwana kama nitajisukuma kufanya mambo mema bila upendo (1 Kor 13:1-3).

Yesu alipoulizwa kuhusu Amri iliyokuu kupita zote alieleza kwa ufasaha kuwa ni upendo kwa Mungu na kwa jirani (Matahyo 22:36-38). Yesu kwa mafundisho yake hapa aneleza kuwa upendo ukitawala nafsi, hausukumwi na hofu wala wajibu na wala hauoni mzigo kufanya mema au kufanya kazi ya Mungu. Ni upendo ulio juu ya amri na maagizo yote. 

 Mafundisho na kushika amri za Mungu hakupaswi kufanywa kwa kutiana hofu au wajibu bali kufundishwa zaidi kwa upendo. Badala ya kutia hofu ya moto wa jehanamu katika kuwasihi watu kutenda mema, ni vyema zaidi kuonesha uzuri wa upendo na ubaya wa dhambi kwa Mungu na kwa jirani. Upendo na ushinde hofu na wajibu.

Yamkini tunaogopa sana hasira ya Mungu kuliko kuutafakari upendo wake. Tunashindwa kuelewa aliposema Ndimi Bwana Mungu wako usiabudu miungu wengine, alisema kwa upendo kwa kuwa anatambua adha tutakayopata tukimpa mgongo yeye, hakusema kwa kujitweza. Kila amri iliyotamkwa na Bwana ina sauti ya upendo, sauti ambayo tutaisikia kama tukianza kuzitazama amri za Mungu kama neno la upendo na si sheria ya kutuhukumu.

Mungu hupendezwa na moyo uliopondeka. Moyo uliopondeka haupatikani kwa kuhofia adhabu bali kwa upendo mkuu. Hofu ya Mungu haipaswi kuwa hofu ya adhabu ya mwisho, bali hofu ya Utakatifu wake na nguvu yake kuu. Tunapomsujudu, tunamwabudu katika Utakatifu na kweli yake. Kumwabudu Mungu kwa roho na kweli kunakuja iwapo ndani mwetu tuna upendo unaozidi uoga wa adhabu na kufanya ibada kwa kutimiza wajibu.

Ukizitazama amri za Mungu, za kanisa na miongozo kama sheria, utafungwa zaidi na sheria si upendo. Utakwenda kanisani au jumuiya kwa uzito na kujivuta kwa kuwa unakwenda kushika amri. Utatoa zaka na sadaka kwa uzito na manung’uniko makubwa kwa kuwa unatoa tu kwa ajili ya kutimiza wajibu na wala sio kwa upendo. Usishangae kusikia mtu akilalama kuwa michango imezidi kanisani.

Katika siku za karibuni hali imekua mbaya zaidi. Hofu na Wajibu hutumika kufanya neno la Mungu kuwa biashara. Badala ya kuwasogeza watu kwa Mungu kwa sauti za upendo vitisho hutumika zaidi. Watu wanalazimishwa kuamini kuwa ukiona haufanikiwi kimaisha au mambo yako hayaendi vizuri ni Mungu anakuadhibu au Mungu amegeuza uso wake hakutazami. Tunajengewa dhana kuwa ukitoa sadaka kubwa ndivyo baraka zako zinavyokua kubwa. Katika muktadha huu, tunawaangalia vipi watu wa hali ya chini na kipato duni? Je, wagonjwa walio mahututi vitandani ni wadhambi sana au hawatoi sadaka?

Injili ya hofu na wajibu inapohubiriwa kwa sauti kubwa zaidi ya mafundisho ya upendo, tunashindwa kuwasogeza watu karibu zaidi na Mungu na wenzao. Ni vyema kuwafundisha watu kutoa sadaka, zaka, kushiriki matendo ya huruma, ujenzi wa nyumba za Mungu na kuwatunza watumishi wa Mungu kwa upendo na si kwa kuwatengenezea hofu na kuwasukuma kwa wajibu. 

Tunapotumia muda na nguvu kubwa kuwaeleza watu juu ya hukumu ya mwisho na moto wa jehanamu, hatuwasaidii sana kama tutakavyowaeleza zaidi juu ya upendo na rehema za Mungu. Namna ambavyo Mungu aliupenda ulimwengu na kumtoa mwanae yashawishi zaidi mtu kumpenda Mungu zaidi ya kumwambia usipompenda Mungu yeye atakuchoma na moto.

Kwa makala hii sisemi kuwa ni vibaya kueleza habari za siku ya mwisho na adhabu za kutotii amri za Mungu, hasha, naeleza juu ya nguvu kubwa ielekezwe wapi. Naeleza kuwa akili na mioyo yetu isifungwe kwa kuogopa adhabu bali isheheni upendo mkuu kwa Mungu na kwa jirani.

Hofu na Wajibu hufanya upendo wetu kwa Mungu na jirani kutokukamilika. Nawasihi ndugu waamini wenzangu, kujifunza zaidi namna ya kumpenda Mungu na jirani, badala ya kujilazimisha kutenda mema kutokana na uoga, hofu na kutimiza wajibu

Benedict Temba
255 712 135 209
benedict.temba@gmail.com

Popular posts from this blog

IFAHAMU SAKRAMENTI YA KITUBIO/UPATANISHO

IFAHAMU SALA YA BWANA (BABA YETU)

NYIMBO ZA BIKIRA MARIA