IFAHAMU SAKRAMENTI YA KITUBIO/UPATANISHO
- Maana
Sakramenti ya kitubio pia huitwa sakramenti ya Upatanisho, ipo katika fungu la sakramenti za uponyaji. Kuna Sakramenti mbili za uponyaji, kitubio na mpako mtakatifu wa wagonjwa. Dhumuni haswa la Sakramenti ya uponyaji ni kuzirejeshea uhai roho zetu pale zinapougua kwa kutenda dhambi. Yesu ndiye tabibu mkuu wa roho zetu naye yu tayari kututibu kila tunapougua. (Katekisimu Katoliki 1420,1421)
Sakramenti ya kitubio huhusisha, kutambua makosa, kujuta na kuungama pamoja na kuweka nia ya kutotenda dhambi hiyo tena.
Kitubio hutusafisha dhambi tulizozitenda baada ya ubatizo. Tunakumbuka, siku ya ubatizo tulipewa kitambaa cheupe, ikiwa ni ishara ya kuwa sasa tumekuwa wapya. Lakini kadri tunavyosongwa na mambo ya dunia, kitambaa chetu cheupe kinachafuka nacho chahitaji kusafishwa, ndio maana tunapata Sakramenti ya kitubio.
- Wakati gani unahitaji Sakramenti ya kitubio
Kila wakati unapotenda dhambi unahitaji Sakramenti ya kitubio. Usisubiri ukirundika dhambi zako ili uungame baada ya mwezi au kipindi cha kwaresma tu. Kila unapohisi umetenda dhambi kimbilia katika kiti cha kitubio kuomba kupatanishwa na Mungu. Tukumbuke kuwa Dhambi inatutenga na Mungu nayo inatuweka mbali na baraka zake, hivyo si vyema sana kukaa katika hali ya dhambi kwa muda mrefu.
- Unaipataje kwa ukamilifu Sakramenti ya Kitubio?
Ili uweze kupata Sakramenti ya kitubio kwa ukamilifu, lazima upitie sehemu kuu mbili
- Mangamuzi binafsi ya ndani ya kutambua kuwa umetenda dhambi, lazima kwanza ujute wewe binafsi ndani ya roho yako ujue ya kuwa umemkosea Mungu. Unapojuta dhambi pia weka kusudi la kuiacha dhambi hiyo. (Bonyeza Hapa kusoma makala ya Toba ya Daudi)
- Jongea kiti cha kitubio kwa ajili ya kuungama dhambi zako kwa Padre. Tunatambua kuwa mitume ndio waliopewa uwezo wa kuondoa dhambi (Yohana 20:23, 2 Wakorintho 5:18). Hivyo mapadre wakiwa waandamizi wa mitume ndio wenye uwezo wa kuondoa dhambi. Unapokwenda kwa Padre kuungama, baada ya kukuondolea dhambi hukupa malipizi ya kufanya (Mfano kusali sala fulani, kushiriki matendo ya huruma au kutoa sadaka). Ni muhimu sana kutimiza malipizi hayo
- Je, umesahau namna ya Kuungama?
Ukifika katika kiti cha kitubio unasema"Padre unibariki kwa kuwa nimetenda dhambi"Padre atakubariki kisha utaendelea ukisema
"Namuungamia Mungu Mwenyezi, nawe Padre wangu, sijaungama tanngu (.....taja mara yako ya mwisho kuungama...)Kisha eleza dhambi zako waziwazi, bila kuficha na eleza umezitenda mara ngapi, ikiwezekana na namna ulivyozitenda. Kuzitaja dhambi zako inakusaidia kujuta kwa mara ya pili juu ya makosa uliyomtendea Mungu.
Baada ya hapo, msikilize Padre, atakuambia usali sala ya kutubu, kisha atakuondolea dhambi zako, akimaliza atakupatia malipizi. Hakikisha unatimiza malipizi.
- Matunda ya Sakramenti ya Kitubio
Baada ya kuungama tunarudi tena katika kundi la kondoo. Ni furaha kubwa sana mbinguni, malaika wanashangilia, kwa maana tulikuatumepotea ila sasa tunarudi.
Tunapatanishwa tena na Mungu, vivyo hivyo tunapatanishwa tena na kanisa. Tunapata nafasi ya kuweza kuzipata baraka zote tulizozikosa wakati tukiwa dhambini.