Je wewe ni Simeoni wa Kirene? (Tafakari)
Tunasoma katika
Injili ya Mtakatifu Marko 15:21, habari za Simeoni wa Kirene aliyemsaidia Yesu
msalaba. Ni mstari mmoja tu, lakini wenye maana kubwa sana katika Imani. Kanisa
kwa kutambua mchango wa mstari huu mmoja, umetenga kituo cha tano katika Ibada
ya njia ya msalaba, kutafakari fumbo hili kubwa.
Nataka nikukaribishe
tuutafakari mstari na fumbo hili la Simeoni wa Kirene anayemsaidia Yesu
Msalaba.
- Mazingira ya
tukio
Simeoni alikua
anatoka shambani kuelekea nyumbani kwake. Yamkini hakua anafahamu ni jambo gani
linaloendelea wakati ule, au kama alikua anafahamu basi halikua jambo la msingi
sana kwake. Maana kama angekua ni mwamini au mwanafunzi wa Yesu Kristo
asingekua anatokea shambani wakati ule, lazima angekua katika hali ya huzuni na
majonzi. Simeoni yamkini alisogea katika msongamano ule wa safari ya kuelekea Kalivari
baada ya kuona mkusanyiko mkubwa wa watu, ni hulka ya binadamu kupenda taarifa.
Labda alijongea ili kujua ni nini kinaendelea.
Lakini ghafla,
anashurutishwa kumsaidia Yesu kuubeba msalaba. Simeoni anapewa kazi ya
kushiriki adhabu, mateso na machungu na mtu asiyemfahamu. Simeoni anakubali,
labda kwa kufuata amri ya askari lakini pia labda kwa huruma anayoiona juu ya
Yesu ambaye alikua yu dhoofu hali.
Simeoni
anashiriki kazi ya ukombozi kwa kuubeba msalaba pamoja na Kristo, jambo lile
limeweka jina lake katika historia ya kanisa duniani, na limeandikwa hivyo pia
katika mbingu. Je, Simeoni wa Kirene ni zawadi gani atayostahili kubwa zaidi ya
kushiriki katika meza ya Bwana milele?
- Funzo katika
fumbo hili
Simeoni, alifanya
jambo moja la upendo na ukarimu. Hakujua zawadi itakayotokana na msaada ule. Simeoni
alikua anatoka shambani, lazima alikua amechoka. Lakini aliuona uchovu wake
kuwa si kitu mbele ya Kristo aliyekua amevia damu mwili mzima, Yesu ambaye mwili wake umechakaa kutokana na mateso. Tendo lake moja la ukarimu, tena bila kufahamu malipo
yake limempa Simeoni nafasi kubwa sana katika historia, katika kanisa na zaidi
ya yote katika Mbingu.
- Wewe pia ni
Simeoni wa Kirene
Kila wakati
unapokutana na mtu mwenye kuhitaji msaada wako, wewe unakua Simeoni wa Kirene.
Yawezekana umetoka shambani namaanisha ukawa umechoka labda huna fedha, huna
nguvu, umebakiwa na akiba ndogo sana nakadhalika. Yamkini mtu anayehitaji
msaada wako ni hohehahe wa kutupwa na watambua hakuna namna ambavyo anaweza
kukulipa.
Kumbuka Simeoni wa Kirene alibeba msalaba na Yesu akiwa ametoka
Shambani na amechoka haswa. Alibeba msalaba wa mtu anayeenda kufa, hivyo alijua
hatopata chochote, aliubeba msalaba kwa ukarimu na upendo. Vivyo hivyo nasi
katika kuombwa msaada, tusijali kuwa tumechoka wala tusitafute faida gani
tutaipata kutokana na kusaidia. Tuwasaidie watuombao msaada, pamoja na uchovu
wetu, tuwasaidie bila kuangalia wataturudishia nini.
Tuufuate mfano wa
Simeoni wa Kirene.