IFAHAMU SALA YA BWANA (BABA YETU)
Utangulizi
Wanafunzi wa Yesu walimuomba awafundishe kusali kama vile ambavyo Yohana aliwafundisha wanafunzi wake kusali. Naye Bwana akawafundisha sala ambaya inatambulika zaidi kama Sala ya Bwana (kwa sababu Bwana mweyewe ndiye aliyeifundisha) aliwaambia msalipo semeni hivi;
"Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea, usitutie katika vishawishi, Lakini utuopoe na yule muovu"
Nyongeza katika sala ya Bwana, Baadaye katika sala ya Bwana maneno yafuatayo yaliongezwa
"Kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu hata milele Amina."
Ukuu wa sala ya Sala ya Bwana
Sala hii imepokea heshima na hadhi kubwa kwenye kanisa tangu wakati huo mpaka leo. Mababa wa Kanisa katika mapokeo, mfano Mtakatifu Agoustino anasema;
"Zipitieni sala zote zilizo katika maandiko na siamini kama mtakuta humo kitu chochote ambacho hakimo katika sala ya Bwana"
Anaongeza Mtakatifu Thomas wa Aquinas akisema;
"Sala ya Bwana ndiyo iliyo kamili kuliko sala zote. Ndani yake hatuombi tu kile tunachoweza kutamani kwa haki, bali pia kadri ya mpango ambao unafaa kukitamani, hivi ni kwamba sala hii haitufundishi tu kuomba bali pia inaunda shauku zetu zote"
Sala hii zaidi ya yote inatupa mwongozo wa namna ya kuomba kwa Mungu wetu. Ukiitazama inaonesha mfano wa sala iliyobora, yenye kuinua sifa na utukufu wa Bwana, kuomba msamaha na pia kupeleka maombi.
Maana ya maneno "Baba yetu Uliye Mbinguni"
Haya ndiyo maneno ya mwanzo katika Sala ya Bwana, maneno haya manne kwa pamoja yana maana kubwa sana;
- Tunaaanza kuonesha ukuu wa Mungu, tunasema yupo juu ya vitu vyote, hii ni sifa ya Mungu. Japokua tunajua kuwa Mungu yupo kila mahali, tunaposema Baba yetu Uliye Mbinguni, tunasema Baba Yetu uliye juu ya vitu vyote.
- Tunakubali na kukiri kwamba tunaye Baba Mmoja aliye Mbinguni, tunakiri ukuu na uweza wake. Tunaikiri amri ya kwaza ya Mungu kwamba yeye ndiye Mungu wetu.
- Vivyo hivyo tunakubali kuwa sisi tu familia kubwa moja. Ndio maana hatusemi Baba yangu, hivyo tunakiri ushirika wa familia moja ya kikristo. Tunakubali kwamba sisi tumeumbwa na naye nasi tu wamoja
- Lakini tunapomtaja Mungu kama Baba tunamleta karibu zaidi, tunaongea naye kama mwanafamilia mwenzetu pia tunaongea naye kama mwenye nguvu na uweza wa kutusaidia, kama vile tunavyoomba kwa baba zetu wa duniani nao wakatupatia, Baba yetu huyu wa Mbinguni atatupatia zaidi ya baba wa duniani.
- Maneno haya yanafanya mambo makuu matatu kwa wakati mmoja; Tunamuabudu, Tunambariki na Tunampenda ndio maana tunamuita Baba Yetu wa Mbinguni.
Maombi Saba (7) yanayopatikana katika Sala ya Bwana.
Maombi haya Saba yamegawanyika katika makundi mawili makuu. Kwanza ni maombi matatu ya kimungu zaidi haya hutuvutia zaidi kwa Mungu, na sehemu ya pili ni maombi manne ya kibinadamu tunaposali kwa kuomba msaada wa Baba Yetu.
Maombi ya Kimungu;
- "Jina lako litukuzwe" tunalitakatifuza jina tukufu la Mungu. Ieleweke kuwa Mungu pekee ndiye mwenye uwezo wa Kutukuza na kutakatifuza. Tunaposema maneno haya tunaliinua jina lake juu. Tunaingia katika mpango wa Mungu na kulitukuza jina lake
- "Ufalme wako Ufike" Tunaukiri Ufalme wa Mungu wetu wa Mbinguni, vivyo hivyo tunaomba Mungu ashushe na atushirikishe ufalme na neema zipatikanazo katika ufalme wa mbinguni. Tunaziita baraka za ufalmw wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku.
- "Utakalo lifanyike Duniani Kama Mbinguni" Tunayakubali mapenzi ya Mungu, jinsi inavyompendeza yeye tunakubali iwe hivyo, lakini pia tunaomba wokovu wa dunia nzima na ukombozi wetu. Pia tunaomba kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima
Maombi ya Kibinaadamu;
- "Utupe leo mkate wetu wa kila siku" Tunaomba wote kwa pamoja kama ndugu malisho ya kiroho na kimwili. Tunamuomba Mungu atulishe na aishibishe miili yetu pia roho zetu. Mkate hutusaidia kukua na tunapoomba kukua kiroho tunaomba pia kukua kimwili.
- "Utusamehe makosa yetu, kama tunavyo wasamehe na sisis waliotukosea" tunakubali kuwa sisi ni wakosefu nasi tunaomba huruma ya Mungu kutusamehe. Zaidi ya hayo tunakubali kuwa sisi tunawasamehe wengine, vivyo hivyo tunaweka ahadi ya kuwasamehe wengine. Hii ni muhimu sana, na ukisali maneno haya usisali kwa mazoea sali ukimaanisha kuwa nawe unawasamehe wengine.
- "Usistutitie katika vishawishi" tunamuomba Mungu atuepushe na kushika njia inayotupelekea kutenda dhambi, tunamsihi atupe Roho Mtakatifu wa kung`amua kuwa tunaelekea katika dhambi na kutusaidia kuepuka vishawishi hivyo.
- "Lakini utuopoe na yule muovu" Yesu alikwisha mshinda Shetani na akamnyanganya funguo za kuzimu. Tunaposali hapa tunaomba nguvu ya kumshinda ibilisi pamoja na nguvu zote za giza. Tunaomba nguvu za kimungu za kupambana na yule muovu.
Hitimisho:
Tuitukuze na kuipenda sala hii ya Bwana, tunapoisali tuisali kwa taratibu na tupate nafasi ya kutafakari maneno tunayoyatamka maana yana maana kubwa sana. Tusiisali sala ya Bwana kama ngonjera bali tutafakari kila neno linalotoka katika kinywa chetu. Hii itatusaidia kusali kwa ukamilifu.