UNGAMA, TUBU KAMA DAUDI (Uchambuzi wa Zaburi ya 51)



Wataalamu wa fasihi wanaeleza kuwa ushairi au utenzi ni namna ambayo binadamu huitumia kueleza hisia zake za ndani kabisa. Ni katika mwangaza huu napenda nikushirikishe utenzi wa Daudi unaopatikana katika Zaburi ya 51.

Daudi aliandika utenzi huu baada ya kutenda dhambi kubwa iliyokua chukizo kwa Mungu. Daudi alitumia madaraka yake, kutembea na Bath-sheba mke wa Askari wake (Uria), kisha baada ya hayo Daudi alimuua Uria ili kuificha dhambi yake. Mungu alimtuma Nabii Nathani, aende kwa Daudi kumweleza kuwa amechukizwa na dhambi aliyotenda Daudi. Kwa majuto makuu Daudi alilia mbele ya Bwana Mungu akitubu (2 Saweli 11, 12:1-15). Zaidi ya hayo aliiandika zaburi hii tuitumiayo sana katika kipindi hiki cha Kwaresima.



Uchambuzi wa Zaburi hii ya 51 unalenga kutusaidia kuungama na kutubu katika dhati na unyoofu wa moyo, pia hutupatia mambo ya kuzingatia wakati wa kuungama. Mambo haya nikuelezayo ni muhimu kuyafanya wakati unatafakari, kabla ya kwenda katika kiti cha kitubio.

  • Omba Huruma ya Mungu.
Daudi anaanza na maneno
1 "............. Unihurumie Ee Mungu, sawasawa na fadhili zako"
Tunapoungama, tunahitaji huruma ya Mungu, tunatambua kuwa si kwa haki yetu tunakwenda kusamehewa bali kwa huruma yake. Hivyo tujongeapo katika kitubio tujongee tukitambua kuwa ni kwa huruma yake tutapata msamaha.

  • Onesha kwamba umetambua makosa/dhambi yako
Daudi anaendelea akisema;
3 "Maana nimejua mimi makosa yangu, na dhambi yangu i mbele yangu daima"
Lazima tuoneshe kwamba tumetambua makosa yetu, ni ishara ya kujuta, ni ishara ya unyenyekevu. Kutokutambua kuwa tumekosa ni kiburi, na Mungu wetu hapendezwi na kiburi

  • Mueleze Mungu umemkosea
Daudi anasema;
4 "Nimekutenda dhambi wewe peke yako na kufanya maovu mbele ya macho yako"
Tunamkosea Mungu kwa kuwakosea wanadamu, hivyo tunapotubu lazima tuseme kwa kujuta kuwa dhambi tulizozitenda tumekuchukiza wewe Mungu wetu. katika kusema hivyo tunasema kwa sauti ya majuto maana hatukupaswa kumuudhi muumba wetu. 

  • Muombe Mungu akusafishe dhambi
Kwa hisia Daudi anasema;
7 "Unisafishe kwa hisopo nami nitakua safi, unioshe nami nitakua mweupe kama theluji"
10 "Ee Mungu uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu"
Baada ya kuonesha majuto makuu na kutubu dhambi, sasa omba neema na utakaso, omba kuumbwa upya na kusafishwa ili kuweza kuketi chakulani na Bwana.

  • Muombe Mungu akurudishie baraka zilizopotea ulipotenda dhambi
Daudi anamuambia Mungu;
11 "Usinitenge na uso wako, wala roho yako mtakatifiu usiniondolee"
12 " Unirudishie furaha ya wokovu wako;..."
Tunapotenda dhambi roho zetu huwa gizani, hukosa nuru na mwanga wa imani. Tunajitenga na Mungu pale tutendapo dhambi. Ndio maana tunapotubu tunapaswa kuomba tena kuunganishwa na Mungu. Tunaomba kupata tena kibali mbele ya macho ya Mungu.

Zaidi ya hayo, tutendapo dhambi tunakua katika jangwa na hatuna furaha, hivyo tunaposali twamuomba Mungu airejeshe tena furaha iliyopotea ndani ya mioyo yetu. Tunaziomba tena baraka za Mungu katika masiha yetu.

  • Weka Ahadi
Daudi anamwimbia Bwana akisema
13 "Nitawafundisha wakosaji njia zako, na wenye dhambi watarejea kwako"
Jambo hili wengi huwa hatulifanyi. Daudi, alielewa uzito wa dhambi aliyoitenda, akaelewa na hasira ya Mungu iliyowaka juu yake. Alitambua kuwa dhambi kubwa huhitaji sadaka kubwa pia. Anapoomba msamaha mbele ya Mungu, anaweka ahadi pia mbele za Mungu. Anamuahidi kuwa atawafundisha watu njia iliyo njema.

Mfano huu wa Daudi tuuchukue, kwanza tuweke ahadi kwa Mungu kuwa; tutajitahidi kadiri ya uwezo weti kuvishinda vishawishi na kuhakikisha hatuanguki dhambini tena. Vivyo hivyo lazima tuweke ahadi ya ziada, mfano; kwenda kushiriki matendo ya huruma, kupalilia makaburi au kutoa sadaka kwa ajili ya dhambi uliyoitenda.

Hii ni muhimu kwani huonesha majitoleo yako kwa Bwana, vivyo hivyo huonesha ni kwa kiasi gani umechukizwa na dhambi uliyoitenda ndio maana unaomba utakaso mbele za Mungu.

.........................................................

Ukishafanya yote haya, jongea kiti cha kitubio kwa ajili ya kuungama Dhambi.








Popular posts from this blog

IFAHAMU SAKRAMENTI YA KITUBIO/UPATANISHO

IFAHAMU SALA YA BWANA (BABA YETU)

NYIMBO ZA BIKIRA MARIA