Kwaresima: Jifunze, Tafakari juu ya fumbo la Shamba la Mizabibu (Isaya 5:1-7)
Katika Isaya 5:1-7,
Nabii Isaya, anaeleza fumbo fupi kupitia kisa cha shamba la mizabibu.
- Kisa cha Shamba
la Mizabibu?
Anaeleza; Mkulima alikua
na shamba la mzabibu, mahali pa kilimani penye kuzaa sana, kwa kulijali akalipalilia,
akalisafisha, akaweka samadi iliyo nzuri, akalitengenezea na kisima cha maji
ndani yake. Akitegemea kuwa litazaa zabibu zilizo njema na safi lakini likazaa
zabibu mwitu, zabibu chungu. Kisha anauliza akisema; Je, ni jambo gani
nililopaswa kulitenda katika shamba langu la mizabibu na sikulifanya? Mbona
nalipotegemea litazaa zabibu safi limezaa zabibu mwitu?
- Fumbo hili lina
maana gani?
Mkulima ni Mungu,
na shamba la mizabibu ni sisi binadamu kila mmoja kwa nafasi yake. Kazi
aliyoifanya mkulima ya kuliandaa shamba la mizabibu ni zawadi, vipawa, na
talanta ambazo Mungu ametujalia. Zabibu ni matunda yatokanayo na zawadi,
talanta na vipawa ambavyo Mungu ametujalia.
- Fumbo hili lina
uhalisia gani?
Katika maisha
yetu Mungu ametubariki katika namna mbalimbali, kila mmoja kwa namna yake
binafsi. Tumejaliwa uhai, elimu, vipaji, hekima, talanta, umaridadi nakadhalika.
Kutoka katika mambo yote hayo Mungu aliyotujalia anategemea tutoe matunda safi
na yenye kupendeza. Anataka tuifundishe jamii njia yake, tuwasaidie watu kwa
upendo, tushiriki katika uenezaji wa injili, tuwafariji wanaaonewa na
kudharauliwa. Mungu anategemea tutumie zawadi zake katika kumtukuza yeye.
Lakini sisi tumekengeuka, tunatumia zawadi za Mungu kumtukuza shetani.
- Tafakari binafsi
Jaribu kufikiri
kila zawadi ambayo Mungu amekupatia ni kwa namna gani unayoitumia? Jiulize pia
kwa namna ambavyo unayaendesha maisha yako je sifa zinaenda kwa Mungu ama hasha!
- Fumbo hili lina
maana gani katika kipindi hiki
Kipindi cha kwaresima
ni wakati wa kujitafakari na kuangalia wongofu. Tunaalikwa kujitafakari kama ni kweli tunatoa
matunda kulingana na nguvu ambayo Mungu amewekeza juu yetu. Endapo tutang’amua
ya kuwa hatutoi matunda yenye kumpendeza Mungu hima tukimbilie katika kiti cha
kitubio na kuomba toba.
- Tusipobadilika
nini kitatokea?
Majibu
yanaonekana katika Isaya 5:5-6, ataliharibu shamba la mizabibu na ataacha
likanyagwe na hatalitunza tena. Hii ni adhabu kubwa mno, maana Mungu ataondosha
baraka zake juu yako naye atakuacha ukiwa bila rutuba, matokeo yake ni
mahangaiko na mateso makuu. Tusifike huku, tumuombe Roho Mtakatifu atuongoze
vyema na atuasaidie kuishika ile iliyo kweli.