AFYA NJEMA – NINI MAANA YAKE? KUELEKEA MSAMAHA

Fr. Innocent Bahati Mushi OFMCap

Moja ya jambo ambalo ni kama mwiba katika ngozi ambalo sisi binadamu tunaalikwa kulifanya ni kuwasamehe waovu kwa kuwatendea mema, na kuwasamehe hata yale yanaonekana hayasameheki. Tunapenda kusoma masimulizi ya watu waliofanikiwa kusamehe uovu waliotendewa kwa upendo, lakini hali hiyo inapotusibu sisi wenyewe, kinachoendelea ndani yetu ni hasira, chuki, mfadhaiko, tunaishiwa nguvu kabisa kiasi cha kuchanganyikiwa. Tunatumia nguvu nyingi sana kupambana na uovu ule na kutaka kulipiza kisasi.

 AFYA NJEMA – UTAFITI CHUO KIKUU HAVARD

Stadi za maisha na tafiti mbalimbali zilizofanywa Havard University  2001 zinaonesha kwamba kama tunataka kuwa na afya njema, kuishi muda mrefu pasipo msongo moyo na mfadhaiko usio na maelezo, ni lazima tujenge utamaduni wa kuachilia maumizo ya zamani na kuwa na mtazamo chanya juu ya wenzetu hata wale wanaoonekana kuwa ni maadui zetu. Katika wema tunashinda mengi, katika ubaya tunaelekea kuzama katika uovu na uadui, na huko ni kujisumisha wenyewe.

AFYA NJEMA – WHO

Kadiri ya shirika la afya duniani (WHO) kuwa na afya njema kwamaanisha ni zaidi ya kutokuwa na magonjwa ya kimwili, kiakili, kisaikolojia, ila pia kuwa na mahusiano bora kijamii. Afya ya kiakili humaanisha kuwa na fikra njema, mawazo na mtazamo chanya. 

Kuwa na afya ya kisaikolojia kwahusiana na hisia zetu pia. Jinsi tunavyojiona sisi wenyewe, tunavyowaona wengine hususani wale ambao wanatuhusu, tunaoishi nao, jinsi tunavyoutazama ulimwengu wa nje na picha tuliyonayo kuhusiana na ulimwengu wa Kiroho – Mwenyezi Mungu. Ni zaidi pia kuhusu shauku zetu, matamanio yetu, mategemeo, na yanayofanana na hayo. Afya ya kiakili pia ni katika kuona mambo katika uhalisia wake.

AFYA YA KIROHO

 Afya ya roho humaanisha mtu kujielewa kwamba maisha yana maana na malengo, hatupo tupo tu, tumeumbwa kwa mpango na kwa malengo maalumu. Ni kuelewa kwamba katika maisha sisi, sio visiwa, tumejengwa juu ya mahusiano na nafsi zetu, na watu, mazingira na Muumba.

Kwamba maisha yanatudai daima kuwa na matumaini kuhusu yale yajayo na kuwianisha mambo haya na uhalisia wa kile tulicho leo hii. Hili linawezekana kama tunaamini kwamba kuna mwezeshaji na anayetufanya kama tulivyo na huyu sio mwingine, ila Mungu mwenyewe. Hatimaye, maisha ya kiroho ni pamoja na kuelewa kwamba, maisha ni zaidi ya vitu tunavyomiliki, kuviona na kutamani – ni kuhusu ulimwengu wa kiroho – tunu, fadhila na heri za kimungu ambazo zinapaswa kutafsiriwa katika mahusiano yetu na watu wanaotuzunguka.

Popular posts from this blog

IFAHAMU SAKRAMENTI YA KITUBIO/UPATANISHO

IFAHAMU SALA YA BWANA (BABA YETU)

NYIMBO ZA BIKIRA MARIA