MKRISTO USIOGOPE KIFO JIANDAE KWA KIFO CHEMA
Makala hii ni sehemu ya Kitabu cha Kalamu kwa Vijana ambacho kipo katika hatua za mwisho kuchapishwa. Haki zote za mwandishi zimehifadhiwa.
Utangulizi
Kati ya mambo ambayo binadamu
tunayaogopa sana mojawapo ni kifo, mwanadamu anaogopa kifo kwa kuwa kwanza
kinamtenga na familia yake, ndugu, jamaa marafiki ambao amezoeana nao, pili
anaogopa kifo kwa kuwa hafahamu ni wapi anapoelekea, jambo lingine
linalowaogopesha watu juu ya kifo ni kuyaacha mambo ya dunia na raha zake
ambazo amekua akizihangaikia kwa muda mrefu sana, kifo huogopwa pia kutokana na
hukumu kwa wale wanaoamini uwepo wa Mungu na hukumu yake. Mwanadamu anapofariki
huku nyuma huacha majonzi na simanzi kubwa haswa kwa wale waliokua wanamtegemea
na wote ambao kwa namna moja au nyengine walikua wanafaidika na uwepo wake hapa
duniani.
Kifo cha kijana mara nyingi huwa
ni pigo zaidi, maana ujana ni wakati wa mtu kuchanua na jamii huwa imejiandaa
sana kuvuna kutoka kwa vijana, anapofariki kijana jamii huhuzunika zaidi haswa
kijana ambaye alianza kupata mafanikio kiasi na ambaye alikua anaonekana ana ndoto
kubwa za kuzitimiza.
Kifo ni nini?
Maana ya kawaida ya kifo ni
kutengana kwa mwili na roho, wakati mwili unarudi udongoni ulipotwaliwa pia
roho hurudi kwa Mungu ilipotoka (Mhubiri 12:7). Kwa Mkristo Mkatoliki maana
sahihi zaidi ya kifo ni mwanzo wa maisha ya umilele katika nyumba na meza
takatifu ya Bwana. Jambo hili linathibitishwa kaika Mtaguso mkuu wa pili wa
Vatikano, hati yake ya liturjia namba 81 na 82 inahitaji uhusiainisho kati ya
kifo cha mwanadamu na ufufuko wa Bwana katika ibada za mazishi (Misale ya
waumini, Uk 1131).
Kifo kimetoka wapi?
Swali hili ni la msingi sana,
mtume Paulo akiwaandikia Warumi (Rum. 5:12-21), anaeleza kuwa dhambi iliingia
duniani kupitia Adamu; mtu wa kwanza na kwa kuingia dhambi mauti pia yakaingia,
hii ina maana kuwa dhambi ndiyo iliyoleta mauti ulimwenguni, Mungu alimweleza
Adamu wazi kuwa siku atakayokaidi amri yake ya kutokula tunda la mti
aliomwagiza hakika atakufa (Mwanzo
2:17), hii inathibitishwa katika adhabu aliyopewa Adamu (Mwanzo 3:19) kuwa
atakula kwa jasho mpaka siku atakaporudi mavumbini alipotwaliwa.
Kila mwanadamu lazima atakufa
Huu ni ukweli ambao wengi
hatupendi kuusikia, Ayubu katika mateso yake anakumbuka hili na kusema wazi
kuwa kila mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke siku zake duniani ni chache (Ayubu 14:1), kwa kuwa binadamu
wote tumerithi dhambi ya asili kutoka kwa Adamu vivyo hivyo tumeirithi adhabu
ya kifo, na kwa maana hiyo kila nafsi lazima itaonja mauti. Kwa maana hiyo
lazima tukutane na kifo kama tamati ya maisha yetu hapa duniani.
Je tusubiri mauti kwa huzuni?
Hasha! Kwa Mkristu mwenye imani
na matumaini kifo si jambo la kutisha, kwani katika kipindi chake chote cha
maisha duniani anaishi kwa matumaini kwamba siku moja ataungana na Bwana wetu
Yesu Kristo, hivyo hukiangalia kifo kama safari ya kumwendea Yesu katika maisha
ya umilele (Katekisimu ya Kanisa Katoiliki: 1020). Huzuni ya kudumu huwa kwa
watu wasio na matumaini na imani. Maana siku tunayolala katika mauti duniani,
tunaamka katika utukufu kwa Baba yetu mbinguni kwani maisha yetu yote tumeishi
tukingoja kwa matumaini kurudi kwake Bwana wetu Yesu Kristu.
Katika hali ya kawaida ya maisha ya mwanadamu, ndugu,
jamaa au rafiki anaposafiri safari ya mbali ambayo itamchukua muda mrefu kurudi
huagwa kwa huzuni na matumaini. Familia humuaga huku ikimtakia kila la kheri na
huahidi kumwombea arudi salama ili waungane tena pamoja. Huo ndio mfano
unaoweza kufananishwa na kifo cha Mkristu. Sisi sote kwa nyakati tofauti lazima
tufunge safari ambayo itatutenga na ndugu, jamaa na marafiki zetu, watahuzunika
kiasi kwani kwa kitambo kidogo hatutakua nao tena pamoja tukishirikiana katika
mambo tuliyozoea kuyafanya pamoja. Lakini saa yaja ambapo sote kwa pamoja
tutashiriki meza ya Bwana wetu. Na katika kipindi cha kusubiri wakati huo
kufika, tutaendelea kuwasiliana kwa njia ya sala na maombi katika ulimwengu wa
roho.
TUJIANDAE KWA KIFO CHEMA
Kifo huja ghafla
Kifo huwa hakipigi hodi, huja
mara moja na huja ghafla. Lakini kanisa linatupatia zawadi ya sala za kuomba
kifo chema (Tazama sala yenye rehema
kamili saa ya kufa, Misale ya waumini Uk. 1089, Sala 15 za Mt. Brigita wa
Sweden, Mawaridi ya Sala Uk. 22-26. Pamoja na sala nyenginezo). Sala hizi
hutusaidia kujiandaa vyema kukipokea kifo pale kinapokuja. Hutupa matayarisho
ya roho zetu kuingia katika uzima wa milele. Zaidi ya yote hutupa matumaini ya
kuuona uso wa Bwana.
Baada ya kifo ni hukumu
Baada ya roho na mwili kutengana,
mwili hurudi udongoni kwani ndiyo asili yake na roho hurudi kwa Baba ambaye
hapo kabla aliipuliza pumzi yake juu ya udongo na kuufanya kiumbe hai. Roho
inaporudi kwa Mungu hutoa hesabu juu ya matendo yake duniani na huhukumiwa
kutokana na mema na mabaya ambayo ilitenda iliokua duniani (Mathayo 25:31-46).
Hukumu si jambo la kuogopa, ili
ni jambo ambalo lazima tulifahamu tunapokua ulimwenguni. Tusisiseme hatutendi
maovu kwa kuwa tunaogopa hukumu ya mwisho, ila tusitende maovu kwa kuwa tunao
upendo kwa jirani na kwa Mungu. Kutokutenda mabaya kwa sababu unaougopa moto wa
milele ni sawa na kusema kama kusingekuwa na moto wa milele ungetenda dhambi.
Ni sawa na mwanafunzi ambaye husoma na kufaulu kwa sababu ya kuogopa asiposoma
atapata adhabu. Mwanafunzi huyu hatasoma kwa furaha bali kwa machungu. Vivyo
hivyo tunapofikiria kuhusu maisha yetu baada ya kifo, tufikirie kuhusu upendo
wa Mungu na furaha ya kuungana naye. Tunapowasaidia watu tuwasaidie kwa moyo wa
upendo bila kuhesabu kwamba nafanya hivi ili nisiende motoni. Kuyafanya mambo
kwa upendo na unyenyekevu ndiyo maana halisi ya moyo uliopondeka ambao Bwana
anapenezwa nao (Zaburi 51:17)
Tufanikishe kusudi la Mungu kutuleta Duniani
Kila mwanadamu ambaye Mungu
amemleta duniani ana kusudi naye. Kabla ya kuumbwa kwetu na kutungwa mimba
alitujua na alikua ameshaweka mipango mema juu yetu (Yeremia 1:5). Hivyo
tunapoishi duniani lazima kwanza tulitafute, tulifahamu na tukamilishe kusudi
la Mungu kwa sisi kuwapo duniani.
Kila mwanadamu amepewa kusudi la
kuutafuta utakatifu na ufalme wa mbingu akiwa hapa duniani. Katika mafundisho
yake Bwana wetu Yesu Kristo alitilia mkazo kwamba duniani tunapita na tutilie
mkazo kuutafuta ufalme wa mbinguni mengine yatakuja kama ziada (Mathayo 6:33).
Mambo tunayoyafanya duniani
yanakusanywa katika hazina yetu mbinguni. Bwana wetu Yesu Kristo anatuasa
tuitengeneze hazina mbinguni mahali ambapo roho zetu zitakuapo, tena
tusihangaike na hazina za duniani (Mathayo 6:20-21). Hili ni katika kutilia
mkazo kuangalia maisha yajayo badala ya kuangalia maisha ya sasa. Mambo ya
dunia hutupa raha kwa kipindi kifupi, ni makosa makubwa kuchagua raha ya muda
mfupi dhidi ya furaha ya umilele.
Hivyo katika kujiandaa na maisha
ya umilele kila jambo tunaloamua kutenda lazima
tulitende tukiwa na malengo ya kutimiza lengo la kuufikia utakatifu na
ufalme wa Mungu.
Baada ya kutizama lengo hili kuu,
kila mwanadamu ana kusudi mahususi ambalo Mungu amemletea duniani. Kusudi hili
ni lazima kila mmoja wetu alitafute na alifanikishe. Mfano mzuri ni Bwana wetu
Yesu Kristo yeye alitambua ya kuwa kusudi lake kuletwa ulimwenguni ni kuukomboa
ulimwengu katika dhambi kwa njia ya kufa msalabani. Aliishi akitambua kusudi
hili na ndio maana kabla ya kukata roho alisema, “YAMETIMIA” (Yohana 19:30). Yesu anasema neno hili kubwa
akimaanisha yote aliyotumwa, yote yaliyoandikwa na yote yaliyotabiriwa sasa
yametimia. Sura ya 17 ya Injili ya Mt. Yohana ni sala ya Kikuhani ambayo Yesu
anaitolea mbele ya Mungu Baba, muda mfupi kabla ya mateso na kifo chake,
anamueleza kusudi ulilonipa juu ya watu hawa nimelitimiza, sasa Baba umtukuze
mwanao. Zawadi anayopokea Bwana wetu Yesu Kristo kwa kazi kubwa hii ni kuketi
kuume kwa Baba.
Sisi nasi yatupasa kutimiza makusudi
mahususi ambayo Mungu ametuatia. Tunapokiangalia kifo kama njia ya kurudi
nyumbani kwa Baba lazima tuatafakari kuhusu kazi Baba aliyotutuma.
Tunapozisafisha roho zetu kwa njia ya kitubio pia tukumbuke kutimiza majukumu
yetu tuliyopewa na Mungu. Tufanye kila kitu na kila jambo ili wakati wetu wa
kuondoka duniani ukifika tuondoke na tabasamu tukisema “YAMETIMIA”. Yatupasa tuondoke tukiwa hatuna deni; tujitafakari na
tutafute lipi ni kusudi mahususi la sisi kuwamo duniani na tulitimize.
Tukisubiri kifo kwa matumaini
Baada ya kuchambua yote hayo kwa
ufupi na kwa uchache twaweza kubaliana kuwa; kifo ni njia ya mwanadamu kurudi
kwa Baba. Pili, roho ya mwanadamu itahukumiwa kutokana na matendo yake ya
duniani. Tatu, ili tuwe tayari kwa kifo chema yatupasa kujiandaa kiroho,
kimwili na kiakili. Nne, lazima tutimize makusudi ya Mungu kutuleta duniani,
kwanza kusudi la jumla la kuufikia uatakatifu kisha kusudi mahususi la kila
mmoja wetu. Zaidi ya yote tuwaombee ndugu, jamaa, marafiki na wote wasio na
mwombezi ambao wameshatangulia mbele za haki, kama wapo toharani Mungu awapokee
katika ufalme wake. Ni vyema tukitizame kifo kwa matumaini ya kumuona tena
Mungu.
Benedict Temba
0712135209
0682657760
benedict.temba@gmail.com