Neno kwa Vijana

Vijana tukumbuke mitume na manabii wengi walieneza dini na neno la Mungu angali ni vijana, wakiwa wana nguvu na wenye kustawi, nguvu yao hawakuipeleka katika maasi na machukizo kwa Mungu, bali waliutoa ujana wao machoni pa Mungu wakiitenda kazi yake, na wengine walikufa wakieneza dini tena hawakuona maumivu yoyote kwa sababu walifanya kwa mapenzi ya Muumba wao.

Kijana ukiwa bado una nguvu usikubali shetani atumie nguvu yako kumuasi Mungu, Mwili wako usitumike kwa uzinzi wala nguvu yako kwa kuiba kwa kunyang’anya, vipaji vyako visiwe chachu ya maovu kwa kuimba na kucheza isivyompendeza Mungu, kichwa chako na kisitumike kutunga na kuandaa hadithi na michezo yenye uovu. Kumbuka nguvu ya ujana wako yaweza kukupa baraka tele kwa Mungu ukiitumia vizuri bali uitumiapo vibaya itakupeleka katika moto wa milele.

Kijana tazama shetani ameweka maoteo mbele yako, usiinue macho yako kutazama wanawake waliovaa vibaya maana utawaka tamaa na binti usiwe kichocheo cha tamaa, kinywa chako kisitoe maneno machafu na yenye kuudhi bali kiwafundishe wadogo zako njia za Mungu, usiitumie simu yako kusambaza uovu maana huchochea dhambi na maasi, usitizame yasiyompendeza Mungu maana yakikujaa utayatenda kwa mwili wako, wakemee wale wanaomkashifu na kumdhihaki Mungu wasiposikia waombee na jitenge nao wasije kukutia vishawishini nawe ukawafuata.

Kijana idhibiti tamaa na uyachunge matamanio yako ili usianguke dhambini, ni kwa juhudi zako ndipo utafanikiwa, usifikiri kula bila kutoa jasho, usitamani usiyojua yamepatikanaje, utajiri wa mwanadamu ni mmoja tu nao ni uzima wa milele, usiitamani utajiri huu uishao bali ule usioisha. Maendeleo huja polepole jitwike moyo wa uvumilivu, ongeza juhudi na utafanikiwa, ukianguka jiinue mara moja, angalia ulipokosea jirekebishe na usonge mbele. Ogopa uvivu na uukimbie.

Kijana isikie sauti ya mzazi wako kabla haijakuita, ukamsaidie bila yeye kukuomba, wewe una nguvu usikubali akadondoka bali umshike na kumsaidia, jivunie uwepo wake kwani ndio uwepo wako, yashike mazuri akuambiayo uyafunge moyoni mwako na uwaambie na wana wako, ukikosana naye mlilie hima akusamehe, akikuudhi usiseme lolote baya juu yake, muombe Mungu amuongoze na akufundishe kupitia yeye.



Kijana eneza upendo, usitende kwa hila, usimsengenye mwenzako tena usimuonee kijicho, akianguka usimcheke kimbia hima umuinue, akichekwa mtie moyo, akifadhaika umfariji, upatapo chakula usile kwa kificho bali na wale wenye njaa, uwaamue waonewao, usishabikie ugomvi bali inuka na uuzime mara moja.

Popular posts from this blog

IFAHAMU SAKRAMENTI YA KITUBIO/UPATANISHO

IFAHAMU SALA YA BWANA (BABA YETU)

NYIMBO ZA BIKIRA MARIA