IFAHAMU JUMATANO YA MAJIVU
“Rarueni mioyo yenu wala si mavazi yenu....”
Yoeli 2:13
UTANGULIZI
Jumatano ya
majivu ni mwanzo wa kipindi cha kwaresima katika kanisa. Ni ishara ya kuanza
kwa siku arobaini za kutafakari kwa undani fumbo kuu la upendo wa Mungu linalofunuliwa
kwa kujitoa kwake na kufa msalabani, kifo cha aibu ili kuichukua aibu yetu. Mama
kanisa anatupatia kipindi hiki ili tuweze kutafakari njia na mienendo yetu.
KWA NINI TUNAPAKWA MAJIVU?
Majivu ni ishara
ya majuto, nayo hufanywa visakramenti kwa kubarikiwa na kanisa. Tunapopakwa majivu
katika paji la uso hutusaidia kutafakari na kutukumbusha kuwa wanadamu sisi tu
mavumbi na mavumbini tutarudi. Hutukumbusha zaidi kuwa maisha ya hapa duniani
tunapita na safari yetu itakamilika pale tutakapoungana na Bwana na mwokozi
wetu katika ufalme wako.
Angalia; Isaya
61:3, Ester 4:1-3, Yeremia 6:26, Ezekieli 27:30, Mathayo 11:21 na Luka 10:13
KWA NINI MAJIVU YAPAKWE KATIKA PAJI LA USO NA SI PENGINEPO?
Ishara yoyote
iwekwayo katika paji la uso huonesha umiliki (soma Ufunuo 7:3, Ufunuo 9:4,
Ufunuo 14:1, Ezekieli 9:4-6, ). Tunapochorwa ishara ya msalaba katika paji la
uso ni ishara kwamba sisi tupo chini yake yeye aliyekufa msalabani kwa ajili
yetu.
Hali kadhalika
hutukumbusha ishara ya msalaba tuliyochorwa na mafuta matakatifu siku ya
ubatizo wetu, hutukumbusha ahadi tuliyoiweka siku hiyo ya ubatizo na kutuita
tuishi maisha ya utakatifu
MANENO ANAYOTAMKA PADRE YANA MAANA GANI?
Tunapopakwa
majivu Padre husema; Mwanadamu kumbuka u mavumbi na mavumbini utarudi AU Tubuni
na kuiamini Injili.
Maneno haya kwa
upande mmoja hutukumbusha tunapoelekea, tusisikitike kwamba siku moja tutarudi
mavumbini bali tuwe na furaha kwani wakati miili yetu unarudi mavumbini roho
zetu zitakwenda kuungana na Mungu Baba mbinguni.
Hivyo maandalizi
tunayoalikwa kuyafanaya si maandalizi ya kuelekea mavumbini bali maandalizi ya
kuelekeza roho zetu mbinguni. Ndio maana pia twaambiwa tubuni na kuiamini
Injili.
MAJIVU HUTOKA WAPI?
Majivu
tunayopakwa hutoka katika matawi yaliyotumika katika jumapili ya matawi ya
mwaka jana. Majivu haya hubarikiwa na kuwa visakramenti. Hivyo majivu
yanapoashiria toba na majuto pia hutukumbusha wema wa Mungu na utayari wake wa
kutusamehe.
KWA NINI TUNATUMIA MATAWI YA JUMAPILI YA MATAWI?
Matawi haya
yalimkaribisha Yesu Yerusalemu akiwa tayari kufa kwa ajili ya dhambi zetu,
yalimpokea mfalme kwa furaha na shangwe kuu. Matawi haya yanapochomwa na sisi
kupakwa majivu yetu yanatukumbusha kuwa ni kwa ajili ya dhambi zetu Mungu
alimtoa mwanae wa pekee kufa msalabani kwa ajili ya dhambi zetu sisi wanaadamu.
Hivyo hututafakarisha kuacha dhambi.