ZINGATIA HAYA UNAPOFUNGA KWARESIMA
Utangulizi
Moja kati ya
mambo yanayoambatana na kipindi cha Kwaresima ni kufunga. Pamoja na hili pia
kuna kusali, kutoa sadaka, kufanya toba na kushiriki matendo ya huruma. Katika kipindi
hiki waamini tunaalikwa kufunga kama sehemu ya majuto na toba kutokana na
dhambi zetu tulizozitenda. Katika maana
pana kufunga ni moja kati ya njia za kutafuta ukaribu zaidi na Mungu. Kufunga
ni kujinyima chakula, maji, vitu au mambo ya kidunia kwa utukufu wa Mungu.
Sheria juu ya kufunga
Ni Amri ya kanisa
kufunga siku ya Jumatano ya majivu na kutokula nyama siku ya Ijumaa kuu. Vivyohivyo
katika sheria za kanisa, sheria namba 1250 mpaka 1252 zinaeleza kuwa Ijumaa
zote pamoja na kipindi cha kwaresima ni siku za toba. Vijana wa kuanzia umri wa
miaka kumi na minne mpaka wazee wa umri wa miaka sitini wana wajibu katika
kanisa wa kufunga na kujinyima katika siku hizo za toba. Ungalizi wa kanisa na
wazazi unahitajika kuwaeleza watoto maana haswa ya kufunga. Hali kadhalika
wazee, wajawazito, wagonjwa pamoja na watu wenye mahitaji maalum hawabanwi na
sheria hizi.
Mambo yafuatayo
ukiyazingatia utapata thawabu katika kufunga kwako
Funga
ukiwa umweka nia, usifunge kwa kuwa ni sheria.
Ni kosa kubwa
kuamua kufunga kwa kuwa tu hiki ni kipindi cha kwaresima kila mtu anafunga nawe ukaamua
kufunga. Kufunga kunahitaji kwanza kuweka nia, kutambua kwa nini unafunga.
- Je unafunga kuomba msamaha?
- Au uanfunga kwa ajili ya kupeleka maombi maalum?
- Au unafunga ili upate ukaribu na kusikia sauti ya Mungu?
- Au unafunga ili upate wasaa wa kutafakari na Mungu ukuu wake katika katika maisha yako?
- Nakadhalika
Hakikisha una nia
madhubuti ambayo unataka kuitimiza usifunge kwa kufuata mkumbo, maana kufunga
kwako hakutakuwa na maana.
Ukishaweka nia yako hii ya kufunga, mshirikishe Mungu na uombe msaada wa Mama Bikira Maria kukusaidia katika kufunga na kuitimiza nia yako.
Kufunga
kunaenda na sala.
Unapoamua kufunga
unatengeneza ukaribu na Mungu, naye yupo tayari kukusikiliza muda wote. Hivyo
unapofunga ni wakati wa kusali sana, ni wakati wa kuzungumza na Mungu.
Unapoianza siku, mueleze Mungu katika maombi ni kwa nini unafunga na umuombe
akusaidie katika kufunga kwako, katikati ya siku mkumbushe Mungu na hata jioni
unapoihitimisha funga yako mshukuru Mungu kwa kukusaidia kuhitimisha salama.
Na usalipo
usisali sala ya kibinafsi, usipeleke maombi yako peke yako kwa Mungu. Omba kwa
ajili ya ulimwengu mzima, Sali pia kwa ajili ya wale wasiomjua Kristo bado,
vivyo hivyo sali pia kwa ajili ya wale wasio na mwombezi.
Kufunga
Kunaenda na Ibada.
Ili funga yako ya
kwaresima ikamilike lazima iambatane na ibada mbalimbali zinazotolewa na
kanisa. Ibada hizi hujumuisha Njia ya Msalaba, Kuabudu Ekaristi, Rozari
takatifu, Ibada ya Misa takatifu nakadhalika. Ibada hizi hukusaidia kukusogeza
karibu zaidi na Mungu, nazo hukupa nafasi ya kumtafakari Mungu katika mafumbo
yake makuu na ya kustaajabisha.
Kufunga
huendana na Tafakari.
Kama nilivyoeleza
awali kuwa unapofunga lazima ujiwekee lengo. Hivyo wakati unaendelea na mfungo
mara kwa mara lazima ufanye tafakari juu ya lengo lako ulilojiwekea. Je, kuna
maendeleo yoyote, kama hakuna maendeleo tatizo ni nini? Pia tafakari juu ya
kufunga kwako kama uanenda sambamba na jinsi ambavyo kanisa linawaelekeza
waamini kufunga.
Kufunga
huenda na toba na kusamehe.
Yamkini lengo lako kuu la kufunga sio kutubu, labda kuna maombi maalumu
unataka kuyapeleka kwa Mungu lakini kabla ya yote unapaswa kwanza kujichunguza
na kufanya toba pamoja na kuwasamehe wale wote ambao wamekukosea. Ukifanya
hivyo funga yako pamoja na maombi vyote vitapokelewa kwa Mungu.
Usifunge
kama wanafiki.
Yesu mwenyewe katika Mathayo 6:13-18 anawaonya wanafunzi wake kwamba
wafungapo wasiwe kama wanafiki ambao hukaa na nyuso za kukunjamana kuonesha
kuwa wamefunga. Kumbuka kuwa unatafuta ukaribu na Mungu, yeye aliyesirini
anayeona moyo wako. Ukijionesha kwa watu ili upate sifa haifai kitu. Kumbuka
kuwa lengo lako la kufunga halikua kujionesha kwa watu.
Kufunga
kuna ambatana na sadaka na matendo ya huruma.
Unapofunga unajinyima na kujikatalia kwa Utukufu wa Mungu, kiasi ya fedha
unachoacha kutumia si mali yako. Hivyo ili funga yako ikamilike kiasi hicho
inabidi ukipeleke madhabahuni kama sadaka au uende ukafanye matendo ya huruma.
Endapo utaitumia fedha uliyoipata kwa kutonunua mahitaji yako wakati umefunga
ni sawa na kuwa uliahirisha kujistarehesha kwa kipindi fulani wala si kwamba
ulifunga.
NIKUTAKIE MFUNGO MWEMA
Je kuna jambo ambalo unadhani ni muhimu kuongezwa katika orodha hii AU kuna
jambo ambalo ungependa niliandikie; Usisite niandikie kupitia benedict.temba@gmail.com au nitumie
ujumbe kwenye 0712135209 nami nitawashirikisha wengine